Pages - Menu
▼
▼
▼
Jumatano, 19 Septemba 2018
HISTORIA YA MKOA WA MTWARA
UTANGULIZI
Mfumo wa utawala wa ukoloni uliigawa Tanzania katika Majimbo 8, Mkoa wa Mtwara ulikuwa ndani ya Jimbo la Kusini ambalo lilijumuisha Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara ambapo Makao Makuu ya Jimbo yalikuwa Lindi.
Mkoa wa Mtwara ulianzishwa rasmi mwaka 1971 kutokana na Mpango wa Madaraka Mikoani ulioasisiwa na kusimamiwa na Rais wa Tanzania kipindi hicho ndugu Julius .K. Nyerere ambao ulilenga kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Mkoa huu ulipoanzishwa ulikuwa tayari na Wilaya tatu (3) ambazo ni Masasi iliyoanzishwa mwaka 1928 chini ya ukoloni wa Kijerumani, Newala iliyoanzishwa mwaka 1956 chini ya wakoloni wa Kiingereza na Mtwara ilianzishwa mwaka 1961.
Kutokana na ongezeko la watu na kukua kwa Mkoa wa Mtwara ziliongezeka Wilaya nyingine 2 ambazo ni Wilaya ya Tandahimba iliyoanzishwa mwaka 1995 kutoka kwenye Wilaya ya Newala na wilaya ya Nanyumbu ilianzishwa
mwaka 2006 kutoka Wilaya ya Masasi.
Kiutawala Mkoa umegawanyika katika Wilaya 5 na Halmashauri 8, Tarafa 25, Kata zaidi ya 159, Vijiji 738, Vitongoji zaidi ya 3,126 na Mitaa isiyopungua 90. Aidha, Mkoa una halmashauri Tatu(3) za mamlaka ya miji ambayo ni halmashauri ya Mji wa Mtwara Mikindani, halmashauri ya mji wa Masasi na halmashauri ya mji wa Newala.
MAANA YA NENO MTWARA
Neno Mtwara limetokana na neno la lugha ya Kimakonde “kutwala” ikiwa na maana ya kuchukua (kunyakua) kitu chochote.
Mtwara ni Jina inalotumika kwa maana 3 tofuati zifuatazo:
• Mtwara jina la Mkoa.
• Mtwara jina la mji wa Makao Makuu ya Mkoa.
• Mtwara ni Wilaya na Makao Makuu ya Wilaya ambayo kiutawala ina Halmashauri 2, ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani na Halmashauri ya Mtwara.
Kutokana na sensa ya taifa watu na makazi ya mwaka 2012 Mkoa wa Mtwara ulikuwa na jumla ya watu millioni moja laki Tatu na elfu ishirini na nne(1,324,000). Mkoa wa Mtwara una makabila makuu 3 ambayo ni Wamakonde wanaopatikana katika
Wilaya za Mtwara, Tandahimba na Newala, Wayao na Wamakua wanaopatikana katika Wilaya za Masasi na Nanyumbu. Kihistoria makabila haya, hapo awali yaliishi pamoja na makabila mengine kaskazini mwa mto Ruvuma. Makabila hayo yaliacha makazi yao na
kukimbilia Msumbiji kutokana na uvamizi na vita vya makabila kutoka kaskazini mwa Tanganyika. Katika kuishi Msumbiji matarajio yao ya kuishi kwa amani na utulivu yalitoweka kutokana na kuibuka kwa vita vya Wazulu. Vita hivyo vilisababisha makabila hayo kurudi ng’ambo ya mto Ruvuma yalikokuwa zamani. Baada ya kuvuka mto Ruvuma,
Wamakonde, Wayao na Wamakua walitafuta maficho hadi kufikia katika bonde la Mkatahumbo na Chitandi. Walitulia katika maeneo hayo ili kuondokana na wasiwasi wa
kukamatwa na Wazulu.
MAHALI MKOA ULIPO
Mkoa huu upo Kusini kabisa mwa Tanzania. Kijiografia upo kati ya Longitudo 38° na 40° Mashariki ya Griniwichi, na kati ya Latitudo 10° 05”na 11° 25” kusini ya Ikweta, na una eneo
la Kilomita za mraba 16,720 ambayo ni sawa na asilimia 1.9 (1.9%) ya eneo la Tanzania Bara ambalo ni kilomita za mraba 885,987. Takribani asilimia 3.91 (hkt 65,450) ya eneo la Mkoa lipo chini ya hifadhi mbili za wanyama ambazo ni Msanjesi (hkt 44,425) na Lukwika/Lumesule (hkt 21,025).
Mkoa wa Mtwara kwa upande wa Kaskazini umepakana na Mkoa wa Lindi, upande wa Mashariki umepakana na Bahari ya Hindi, upande wa Kusini kuna Mto Ruvuma unaotenganisha Tanzania na Msumbiji, wakati upande wa Magharibi umepakana na Mkoa wa
Ruvuma.
HALI YA HEWA
Mkoa wa Mtwara una vipindi viwili vikuu vya majira. Majira ya mvua ambayo huitwa masika na majira ya ukavu ambayo huitwa kiangazi. Hakuna mvua za msimu maalum kama vile za Vuli zinazopatikana sehemu nyingine Tanzania. Kwa kawaida Mkoa wa Mtwara
hupata mvua ya wastani wa mm 935 hadi 1,166 kwa mwaka. Wilaya inayoongoza kupata mvua nyingi ni Newala ambayo hupata wastani wa mm.1001, Wilaya inayopata mvua kidogo ni Nanyumbu ambayo hupata wastani wa mm.832.
Kwa kawaida kiwango cha juu cha joto Mkoani Mtwara ni 32C mwezi Disemba na kiwango cha chini cha joto huwa ni 28C mwezi Julai.
AINA YA UDONGO
Udongo hutegemea hali ya jiolojia. Katika Mkoa huu kuna kanda mbili za kijiolojia. Kwanza ni ukanda wa pwani ambao unaendelea kwa kilomita 125 kutoka bahari ya Hindi hadi ukanda
wa Makonde ujulikanao kama Makonde plateau uliopo Newala. Ukanda huu udongo wake ni wa kichanga na wenye rutuba hafifu na uwezo mdogo wa kushikilia maji. Maeneo mengine katika ukanda huu yana udongo mzito
wa aina ya mfinyanzi. Vilevile mawe ya chokaaa yaliyopo pwani hutoa udongo mwekundu unaopitisha maji vizuri.
Ukanda wa pili wa kijioliojia huendelea Magharibi ya ukanda wa pwani, ukanda huu una asili ya mawe yaliojishindilia kwa chini. Kaskazini ya mji wa Masasi kuna udongo wa mfinyanzi uliochangayika na udongo mwekundu, udongo huu ndio bora kuliko aina zote kwani ndio
unaofaa kwa mazao ya chakula na biashara.
Usikose kusoma Sehemu ya Pili....
Unaweza kutoa maoni au ushauri au kuulizia historia ambayo ungependa iwepo katika sehumu ya pili ya historia ya mkoa wa Mtwara kwa kuandika comments yako.
Chanzo: Mtandao(websites and internet), takwimu taifa na Cosmas Pahala(Masasi).